Wednesday, February 08, 2017

Mahakama yawataka mawakili wa utetezi katika kesi ya kina Mpemba kuacha lugha tamu tamu kana kwamba kesi yao imeiva.

Mahakama imewataka mawakili wa utetezi katika kesi ya kukutwa na nyara za serikali zenye thamani ya sh. Milioni 785.6 inayomkabili Yusufu Yusufu maarufu kama Mpemba kuacha kuwaeleza washtakiwa lugha tamu tamu kana kwamba kesi yao imeiva.

Hakimu Mkazi Thomasi Simba wa mahakama ya hakimu Mkazi Kisutu aliwaambia mawikili hao kuwaeleza ukweli washtakiwa na siyo kuwapa lugha tamu wakati wakijua fika safari yao bado ni ndefu na mbele kuna shubiri.

Hatua hiyo ilikuja wakati kesi hiyo asubuhi ilipofika mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa na Wakili wa serikali Elia Athanas kuieleza Mahakama kuwa jalada la kesi liko kwa RCO.

"Mheshimwa kesi leo imekuja kwa ajili ya kutajwa lakini jalada bado liko kwa RCO kwenye utaratibu wa kuandaliwa vijarada mbali mbali kwa ajili ya kupeleka mahakama ya mafisadi.

Lakini kabla kesi haijaahirishwa mawakili wa utetezi wakiongozwa na Nehemia Nkoko waliwataka Jamhuri  kumpa presha RCO ili amalize kuandaa hayo majarada na kesi iende mahakama ya mafisadi.

" kutokana na kauli za jamuhuri inaonekana kuwa upelelezi haujakamilika tu naomba wawe na kauli moja kuwa upelelezi bado", walisema.

Baada ya hoja hizo hakimu Simba aliwataka mawakili wawe wawazi kwa washtakiwa, waache kuwafanya wajue  kwamba jalada likitoka kwa RCO linarudi moja kwa moja mahakamani wakati wanajua fika kuwa ni lazima liende kwa DPP kisha Kisutu kwa Committal tayari kwa kwenda mahakama ya mafisadi.

"Safari bado ni ndefu sana kwa washtakiwa, acheni kuwaeleza lugha tamu tamu wakati unajua mlolongo mzima" alisema hakimu Simba

Awali, upande wa Jamhuri uliiambia Mahakama hiyo kuwa jalada hilo liko kwa Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro analifanyia kazi ili liende ngazi zingine kwa hatua zaidi.

Mkuu huyo akishamaliza kulifanyia kazi atalipeleka kwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Biswalo Mganga kwa hatua zaidi za kulitolea uamuzi atakaoona unafaa katika kesi hiyo

Mbali na Mpemba ambaye ni mkazi wa Tegeta, washitakiwa wengine ni Charles Mrutu (37) wa Mlimba, Morogoro, Benedict Kungwa (40) wa Mbagala Chamazi, Jumanne Chima (30) wa Mbezi, Ahmed Nyagongo (33) dereva na Pius Kulagwa (46).

Washitakiwa hao wanadaiwa kujihusisha na mtandao wa ujangili na biashara ya meno ya tembo yenye thamani ya Sh milioni 785.6.

Ilidaiwa kuwa katika tarehe zisizofahamika kati ya Januari 2014 na Oktoba, mwaka jana wakiwa Dar es Salaam, Tanga, Iringa na Mtwara, walikusanya na kuuza vipande 50 vya meno ya tembo vyenye thamani ya dola 180,000 sawa na Sh milioni 392.8 mali ya Serikali bila kibali cha Mkurugenzi wa Wanyamapori.

Aliendelea kudai kuwa katika mashitaka ya pili, Oktoba 26 mwaka jana washitakiwa wakiwa Mbagala Zakhem, Temeke walikutwa na vipande 10 vyenye uzito wa kilo 13.85 na thamani ya dola 30,000 sawa na Sh milioni 65.4.
Ilidaiwa kuwa katika mashitaka ya tatu, Oktoba 27 mwaka jana washitakiwa wakiwa Tabata Kisukuru, walikutwa na vipande vinne vyenye uzito wa kilo 11.1 na thamani ya dola 15,000 sawa na Sh milioni 32.7.

Pia Oktoba 29 mwaka jana walikutwa na vipande 36 vya thamani ya Sh milioni 294.6.
Kesi imeahirishwa hadi Februari 21 mwaka huu.

No comments: